Monday, 17 June 2013

"MLIPUKO WA BOMU LA ARUSHA ULIPANGWA NA CHADEMA WENYEWE".....NAPE NNAUYE


Itakumbukwa tarehe 16/06/2013 ilikuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa baadhi ya kata nchini. Uchaguzi huo umefanyika kwenye kata ishirini na mbili (22) -kati ya kata ishirini na sita (26) zilizotangazwa kufanya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi wazi.

Matokeo tuliyoyapata toka kwenye maeneo yaliyofanya uchaguzi yanaonyesha kuwa kati ya kata 22 zilizofanya uchaguzi CCM tumeshinda kata 16 sawa na asilimia 72.72% na wenzetu wamechukua kata 6 zilizobaki sawa na asilimia 27.28%.
Tunawashukuru sana kote walikoonyesha imani yao kubwa kwa Chama chetu kwa kutupa dhamana ya kuendelea kuwatumikia. CCM inawaahidi utumishi uliotukuka.
 
 Hata wale 27.28% walioamua kuwajaribu wenzetu, tunawatakia kila lakheri, kwani wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua wanaodhani watawasaidia kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Uchaguzi kwenye kata hizi zote umeisha sasa tuwatumikie wananchi.

Kata nne za jiji la Arusha hazikufanya uchaguzi baada ya kuahirishwa kufuatia tukio la kusikitisha la kulipuka kwa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema mjini Arusha tarehe 15/06/2013.

CCM tunalaani tukio hilo la mlipuko wa bomu na matukio yanayofanana na hayo katika nchi yetu. Tunawapa pole wale wote walioathirika na tukio hilo.
 
Ni vizuri serikali ikalichunguza swala hili kwa kutumia muda mfupi na kuhakikisha waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Pamoja na kulaani na kuitaka serikali kukomesha vitendo hivi nchini, ni wakati muafaka kwa vyama vya siasa nchini kujitazama upya kwani kuna kila dalili kuwa tukio hili kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari mhe. Mbowe Mwenyekiti wa Chadema Taifa kuwa ni la kupangwa, inawezekana limepangwa na Chadema wenyewe.

Hali ya kisiasa jijini Arusha kuelekea uchaguzi huo ilikuwa wazi kuwa wana Arusha walishaamua kuzirudisha kata hizo nne kwa CCM, hasa baada ya kuchoshwa na maandamano na vurugu za kila siku jijini Arusha. 
 

Aidha kauli za kukata tamaa za viongozi wa Chadema na vitendo vyao ni dalili tosha kuwa tukio hili lilipangwa na Chadema wenyewe.

CCM tunaendelea kusisitiza na kulaani juhudi za wenzetu kujaribu kujenga umaarufu wa chama chao juu ya damu za Watanzania. Juhudi hizi zinapaswa kulaaniwa na wazalendo wote ndani na nje ya nchi.
 
 Tukumbuke asiyekubali kushindwa, si mshindani. Si busara wala uungwana na ni kinyume na utu kutumia majanga ya kutengeneza kama mtaji wa kisiasa.

Lakini CCM tunalaani pia kitendo cha viongozi wa Chadema kujaribu kutumia baadhi ya misiba na majeruhi wa tukio hili kisiasa na mwisho wa siku kwenda kuwatelekeza hospitali baadhi yao baada ya kuwaahidi kubeba gharama zote za matibabu na mazishi.
 
Tunaipongeza serikali kwa kuingilia kati na kuwasaidia waathirika hawa na kuhakikisha wanapata huduma inayostahili.

CCM inarudia kueleza masikitiko yake kwa waathirika wa tukio hili la kinyama na kikatili lisilostahili kuvumiliwa hata kidogo. 
 

Kama Chama tumeguswa sana na tukio hili pamoja na kulilaani, tunawasihi watanzania tushindane na kutofautiana bila kupigana na kuvunja tunu ya nchi yetu ya amani na utulivu. 
 

Katika demokrasia ya vyama vingi swala la kuvumiliana ni swala la msingi sana katika kufikia ukomavu wa demokrasia hiyo.

Imetolewa;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi.
17/06/2013

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...