Je, umeshahisi mtu anayehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela
anajisikiaje? Je mtu anayefeli mitihani yake ya form 4 ambapo alijituma kwa
bidii miaka yote 4 lakini akajikuta anafeli ? Je, umewahi kukata tamaa na kuona
maisha ndio yamefika mwisho?. Makala hii
inachambua namna ya kuishi kwa matumaini na kushinda hali ya kukata tamaa.
Niliwahi kuwa jela/gerezani na wafungwa waliokuwa wakitumikia vifungo vyao kwa
miaka kadhaa. Ninaposema jela, namaanisha ndani kabisa ya jela, sio nje kama
vile kumtembelea mfungwa. Nilikuwa gerezani ila sio kama mfungwa bali kama
mwalimu maalum wa wafungwa. Nilistaajabishwa kwa jinsi wanafunzi wangu wafungwa
walivyokuwa na matumaini ya maisha. Kwa jinsi ambavyo wanafunzi wangu ambao ni wafungwa walivyokuwa wakijituma waelewe
nilichofundisha na jinsi walivyokuwa na hamu ya kupata ujuzi ingawa wengi wao
walikuwa bado wanatumikia vifungo kwa miaka mingine zaidi ya mitano.
Novemba 2012,
nilipata nafasi ya kuenda kufundisha wafungwa wakiwa gerezani katika gereza moja
hapa Afrika Kusini. Ilikuwa ni kuwafundisha jinsi ya kutumia program ya uhasibu
iitwayo Pastel. Kwa makubaliano ya gereza hilo na chuo ambacho nimeajiriwa,
ilinipasa kutoa masomo kwa wiki nne mfululizo, mara mbili kwa wiki, na kwa
siku ni masaa 2, ambapo nilieleza
nadharia ya Pastel Parter V11 na kusimamia matumizi kwa vitendo ya hiyo program.
Nilitoa mafunzo ndani ya gereza katika chumba maalum chenye ulinzi mkali.
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia gerezani , niliwahi kuona tuu jinsi ulinzi
mkali ulivyo gerezani, ila safari hii nilishuhudia ‘live’. Kuingia huko
gerezani ilibidi kupitishwa kwenye mageti sita, ambayo yote yalikuwa yana
walinzi waliojizaziti. Baada ya kumaliza somo la siku , nilisindikizwa mpaka
nje ya gereza na kuondoka, kesho yake nilifuatwa chuoni kwa gari maalum la gereza na kuenda
kufundisha , mpaka muda wa mkataba ulipoisha nikaacha kuenda gerezani.
Habari ya kuwa gerezani , uzoefu wa maisha na kujifunza kwa makala na
vitabu mbalimbali kumeniweza kutambua mambo yafuatayo kuwa ni ya msingi kwa mtu
ambaye anajihisi kukata tamaa.
Ni muhimu sana kushinda hali ya kukata tamaa
kwani ina madhara ya kiafya, kiakili na hata wengine huamua kujiua.
Soma mbinu zifuatazo
za kushinda hali ya kujihisi kukata tamaa:-
Nafasi yako katika
kuleta matumaini ya maisha:
Pamoja na kuwa unahitaji watu wengine kukupa
msaada na kushirikiana nao katika mambo kadhaa , wewe kama wewe una nafasi
kubwa zaidi ya hao wote ukiwajumlisha. Mfano katika hali hiyo ya kukata tamaa,
wewe ndie pekee mwenye uwezo wa kuamua kuwa sasa kukata tamaa basi, na badala
yake utafute suluhu ya hilo linalokuumiza, na kama suluhu haiji haraka basi ni
bora kulipuuzia jambo husika, kwani kama hauwezi jambo usiloweza kulipatia
ufumbuzi , hata ukihuzunika, haisaidii kwani wakati huu unapokuwa umekata
tamaa, jambo kubwa unalolihitaji ni ufumbuzi wa hilo tatizo. Hivyo kama ufumbuzi wa tatizo
haupo kwa mujibu wa ufahamu wako, basi ni bora kuangalia njia nyingine kuliko
kuendelea kuhuzunika.
Tengeneza picha kubwa ya maisha:
Unapokata tamaa unaweza
kujikuta ukichukulia kuwa jambo hilo moja linalokufanya ukate tamaa ndio jambo
pekee maishani mwako, na kwakuwa halijaenda vile unavyoona lilitakiwa liende
basi maisha yako hayana thamani tena.
Hata hivyo, fikiria hivi haujui umri wako
hasa wa kuishi duniani kikomo chake ni kipi, pengine maisha yako ni miaka 20 au
30 ijayo , hivyo kukata tamaa kwa jambo hili moja hakufai kwani bado una miaka
mingine mingi ya kuishi na kurekebisha mambo.
Pengine ni jambo moja au mawili
tuu ndio yanakukatisha tamaa ya maisha, mfano ajira, hasara ya biashara, au
kuachwa na mpenzi, hata hivyo ukitengeneza picha kubwa ya maisha utagundua kuwa
maisha yako yanaundwa na mambo mengi sana zaidi ya hiyo ajira inayokukatisha
tamaa, au huyo mpenzi anayekuumiza kichwa, au wateja/wapinzani wanaofanya
biashara yako isiende vyema.
Utagundua kuwa una muda mwingi wa kurekebisha
mambo na kwamba una mambo mengine mengi tuu ya kufanya na maisha yako ukayaendeleza.
Usijilinganishe:
Katikahali uliyonayo ya kukata tamaa,
kujilinganisha na watu wengi kunaweza kuchochea kukata tamaa zaidi kwani siku
zote wapo watu walio na uwezo au nafasi kubwa kuliko wewe, au wenye furaha
zaidi kuliko wewe.
Kumbuka kukata kwako tamaa ni jambo lako binafsi hivyo
inabidi utafute ufumbuzi binafsi na sio kujidimiza kwa kujilinganisha na walio
na hali nzuri zaidi kuliko wewe.
Isitoshe maisha ni safari ndefu , hao unaodhani
walio bora pengine siku si chache watakuwa wapo chini kimaisha kuliko ulivyo
wewe,na zaidi sana kumbuka furaha ni jambo binafsi unaweza kudhani fulani
anafuraha kwa kumtazama kwa nje, au kwa vitu alivyo navyo, ila kumbe kiukweli,
ana huzuni na pengine anakaribia kukata tamaa.
Kumbuka uwezo wako na sio mapungufu yako:
Unajpojisikia
kukata tamaa , kumbuka wewe mwenywe ndio ndio msaada mkubwa katika
kukabiliana na hali hiyo, na njia kubwa zaidi ya kufanikiwa ni kukumbuka mambo
makubwa unayoweza kufanya, na sio madhaifu yako.
Tafuta chanzo (Usijidanganye wala Usijilaumu):
Kulalamika, kujilaumu hakusaidii kutatua
tatizo linalokukabili, au hilo jambo linalokukwaza.
Badala yake tafakari kwa umakini na kwakuwa mkweli wa nafsi yako ili kujua
kwanini hasa tatizo ulilo nalo lipo.
Hali ngumu = Fursa ya kuwa bora zaidi:
Fikiria tatizo lako
kama changamoto ambayo inakupa somo la
nini cha kufanya zaidi ili kurekebisha
hali uliyo nayo. Na zaidi sana, utakapoweza kuondokana na hali husika ya kukata
tamaa, utaweza kuwa na uzoefu ambao utakusaidia katika siku zijazo. La msingi fanya utafiti wa makini wa jinsi ya
kutatua hali husika, na uchukue uamuzi mapema.
Kumbuka fadhila na mafanikio:
Katika hali ya kukata tamaa unawezakujikuta
unasahau mazuri yote yaliyowahi kukutokea katika maisha yako, na kusahau pia
mafanikio ambayo ulikwisha wahi kuyapata katika maisha yako. Tambua kuwa bado una nafasi ya kuendelea
kupata fadhila na mafanikio, kwani uwepo wa tatizo ulilo nalo haimaanishi kuwa
milango yote ya fadhila na mafanikio ndio imefungwa.
Zungumza/Omba msaada:
Usikae kimya na hali yako inayokukatisha tamaa. Tafuta msaada kwa watu
sahihi. Jitahidi kutambua aina sahihi ya watu wa kuwa nao karibu hasa unapokuwa
katika hali ngumu ya kukata tamaa kwani baadhi ya watu watakuongezea kukata
tamaa.
No comments:
Post a Comment