Taarifa
zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk. Willibrod Slaa, zinaeleza kugoma huko kwa Profesa Baregu
kumeilazimisha Chadema kufanya maamuzi ya kuitisha Mkutano wa dharura wa
Kamati Kuu kwa ajili ya kulijadili suala hilo, ikiwa ni pamoja na
kufikia maamuzi ya kichama na hatua za kuchukua.Hivi
karibuni Chadema kilisema kuwa hakiridhishwi na mchakato mzima wa
kutunga Katiba mpya, baada ya masharti kiliyotoa kwa serikali kikitaka
kifanye mabadiliko kutotimizwa, na hivyo kumuagiza mwakilishi wao, Prof.
Baregu ajitoe ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba baada ya
kujitoa kitaanzisha kampeni ya nchi nzima kuwahamasisha wananchi wasusie
mchakato huo.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Chadema ulipingwa na Prof. Baregu mwenyewe,
ambaye alikataa kujitoa kwa hoja kwamba haoni kama kuna mambo
yanapindishwa na serikali ndani ya Tume hiyo kama ambavyo chama chake
kinadai.
Zikiwa zimepita siku tano (jana) tangu muda aliopewa Prof. Baregu na
Chadema kujitoa katika Tume kuisha na yeye kugoma, kimesema kuwa suala
hilo majibu yake yatapatik
ana kupitia kikao cha dharura cha Kamati Kuu kitakachoketi muda wowote kuanzia sasa.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod
Slaa, alisema: “Suala hili alilitoa Mwenyekiti wangu na sina cha
kuongea, nimekuwa najibu swali hili kwa waandishi mbalimbali wa habari,
kwa ufupi jambo hili litazungumzwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Chama.
Sijui muda wala siku kwa sababu bado hakijapangwa.”
Wakati Dk. Slaa akiweka msimamo huo wa chama, baadhi ya wafuatiliaji wa
masuala ya kisiasa wanamshutumu Prof. Baregu kuwa amekataa kufuata
maagizo ya chama chake kwa sababu ya malipo makubwa wanayopatiwa
viongozi na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutokana na wahusika kugoma kuzungumza
zinaeleza kuwa, viongozi na wajumbe wa Tume hiyo kwa siku wanalipwa
kiasi cha shilingi laki tano, ambapo kwa mwezi ni karibu na shilingi
milioni 12-16.
Pamoja na hilo, juzi wakati Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni
wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alipokuwa akiwasilisha
hotuba yake kuhusu mpango wa makadirio ya mapato ya fedha ya Wizara ya
Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, alihoji matumizi
makubwa ya mabilioni ya fedha za wananchi ndani ya Tume hiyo, akidai
kuwa yanaashiria harufu mbaya ya ufisadi.
Alisema matumuzi hayo hayaelezeki wala kukubalika kwa misingi ya kisheria na kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume hiyo.
Lissu alihoji Bunge kuombwa tena kuidhinisha shilingi bilioni 33.944,
kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka jana kwa ajili ya matumizi ya
Tume kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/14.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji
wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya
83 ya Sheria za Tanzania.
Hata hivyo matumizi yake yamezua mashaka na kwa mujibu wa Lissu, kuna ulaji zaidi kwa wajumbe wa Tume hiyo.
Alipoulizwa Prof. Baregu kwamba dhamira ya kugoma kutekeleza maagizo ya
chama chake imesukumwa na fedha nyingi anazozipata kutoka katika Tume ya
Katiba na si utaifa kama anavyodai, alisema anachokifikiria kuhusu tume
hiyo ni kwamba inapewa fungu dogo sana la fedha kuliko tume nyingine
zilizopata kuundwa.
“Unajua kuna habari nyingi za uzushi ambazo zimekuwa zikiinyoshea kidole
Tume hii, hasa wanasiasa wako mstari wa mbele katika hili, mara
utawasikia, Tume tunalipana posho kubwa hadi wengine wanadiriki kusema
tunachukua posho ya Sh. 500,000 kwa siku.
Wengine
utawasikia wanadai tunalipwa mamilioni ya fedha kwa mwezi, laiti kama
wangeufahamu ukweli wasingeweza kutamka maneno hayo,” alisema Prof.
Baregu.
Kuhusu
kukaidi kwake agizo la chama chake kilichomtaka ajiengue kwenye Tume ya
Katiba, Prof. Baregu, alisema hajui kitu chochote kuhusu hilo kwa sababu
hana taarifa zaidi kutoka katika chama chake inayomuelekeza afanye
hivyo.
Aliwataka wanasiasa wasiingilie Tume hiyo, kwa sababu inafanya kazi muhimu kwa muktadha wa maisha ya Watanzania.
“Si
vizuri tukiwa bado kwenye mchakato kuanza kutoka relini, suala la Katiba
ni jambo nyeti na linahitaji mshikamano wa pamoja na si kutishia
kujiondoa katika njia ya kuelekea kupata Katiba Mpya.
“Mimi
kuwa Chadema kunatokana na dhamira yangu, lakini kikubwa ninachokiona ni
kuwasaidia wananchi, hivyo hatuna budi kuungana kwa pamoja ili kuzaa
Katiba yenye kumsaidia kila Mtanzania,” alisema Baregu.
Alisema
yeye katika Tume hiyo ni mtaalamu pekee wa masuala ya Sayansi ya siasa,
hivyo ana ufahamu umuhimu wake ndani ya mchakato wa kutengeneza Katiba
mpya
No comments:
Post a Comment