Asasi inayomtumia Miss huyo, ambaye kwa sasa ni msanii wa filamu nchini kama mmoja wa viongozi wake inajulikana kwa jina la Saving Foundation, yenye makao yake jijini Dar es salaam.
Saving Foundation ambayo imejieleza kwa kina katika website yake ya www.saving foundation loans.com inadai kutoa mikopo isiyo na riba kwa watu mbalimbali kati ya sh. milioni tatu hadi sh. milioni 20 kwa shughuli za kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba bora.
Kabla ya kupatiwa mkopo, mteja hutakiwa kujisajili kwa gharama ya sh. 83,500, hupatiwa namba ya usajili, kisha hujaza fomu ya mkopo sanjari na kulipa ada ya mkopo kutegemea na kiasi cha mkopo alichokiomba, ambapo mkopo wa sh. milioni 20 hulipiwa ada ya sh. 130,000.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa simu mmoja wa viongozi hao aliyejitambulisha kwa jina la 'Wema Sepetu', alisema baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili, kulipa ada ya mkopo, mteja hutumiwa mkopo wake ndani ya dakika 45.
"Mteja hutumiwa mkopo wake ndani ya dakika 45, mara baada ya fedha zake za ada kutufikia ambayo hutumwa kwa njia ya Tigo Pesa au M-Pesa," alisema mmoja wa viongozi wa asasi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la 'Wema Sepetu' alipozungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu.
Namba za simu zinazotumiwa na asasi hiyo kupokea fedha kutoka kwa wateja ni 0715 373 307 iliyosajiliwa kwa jina la Wema Sepetu na 0757 856 966 yenye usajili wa jina la Said Mkama.
Baada ya maelezo ya 'Wema Sepetu' huyo feki wa asasi hiyo, ilibainika kwamba haikuwa sauti ya Wema Sepetu halisi japo muhusika alisisitiza kuwa ndiye yeye.
Baada ya maelezo hayo, mwandishi wa habari hizi alimtafuta Wema Sepetu, halisi ambaye alizungumzia kuhusu asasi hiyo, ambayo alikana kuitambua.
Kuhusu namba ya simu 0715 373 307 iliyosajiliwa kwa jina lake, Wema alisema haijui na hajaawahi kuimiliki, namba yake ya tigo aliyowahi kuimiliki ambayo ni tofaauti kabisa na inayotumiwa na asasi hiyo.
"Sijui chochote kuhusu asasi hiyo, sijawahi kumiliki namba hiyo ya Tigo, hao ni matapeli waliodhamiria kutumia jina langu pengine kufanikisha utapeli wao, nasema kwamba, Wema wa asasi hiyo si mimi, watu wote wawe makini na matapeli hao waliothubutu kusajili namba ya simu kwa jina langu, hawa ni watu hatari," alisema Wema.
Hata hivyo, Wema alikiri kupata taarifa kutoka kwa watu mbalimbali kuwepo kwa watu wanaofanya utapeli kwa kutumia jina lake, lakini hajui cha kufanya zaidi ya kuviachia vyombo vya usalama na kuwadharlisha watu wote kuwa makini na matapeli hao.
Mmoja wa watu waliotapeliwa na asasi hiyo mwaka huu aliyezungumza kuhusu utapali huo ni Wilson Makumila (35), mkazi wa Uwanja wa Ndege, Dar es Salaam na ni mfanyabiashara ndogo ndogo, ambaye alitaka mkopo wa sh. milioni 20 kwa lengo la kujenga nyumba bora, mkopo ambao ili apatiwe alilazimika kutoa jumla ya sh. 213,000 kwa ajili ya kujisajili na ada ya mkopo wenyewe.
"Baada ya kujaza fomu ya mkopo, niliambiwa nilipe sh. 83,500 ili kujisajili, Januari 11 mwaka huu nilituma fedha hiyo kupitia Tigo Pesa kwenda namba 0715 373 30, muda huo huo nilitumiwa namba yangu ya usajili ambayo ni 89654112," alisema Makumila
Alisema, alitakiwa na watu hao kutuma fedha nyingine sh. 130,000 kwa ajili ya ada ya mkopo, watakapoipokea, ndani ya dakika 45 atatumiwa kwa njia ya Tigo Pesa au M-Pesa fedha yote ya mkopo aliyoiomba.
"Kwa siku hiyo sikuweza kutuma sh. 130,000 kwani, sikuwanayo, nilipita kuazima kwa watu nakuituma kwa njia ya M-Pesa kwa siku tatu tofauti kwenda namba 0757 856 966, Januari 14, saa 9:15 sh. 25,000, Januari 15, saa 10:10 jioni sh. 40,000, Januari 16, saa 4:30 asubuhi nilituma kiasi chote cha fedha iliyokuwa imesalia sh. 65,000 na kungoja kwa matumaini kutumiwa ndani ya dakika 45 sh. milioni 20, mkopo nilioumba bila mafanikio," alisema Makumila.
Alisema baada ya kungoja kwa siku nzima bila fedha hiyo kutumwa, alipiga simu kwa viongozi wa asasi hiyo ambao hawakuipokea hivyo, mwishoni mwa wiki asubuhi akalazimika kufunga safari hadi jengo la Utumishi Posta, Dar es Salaam zilipo ofisi za asasi hiyo kama alivyoelekezwa na wahusika.
Makulila alipofika katika jengo hilo alipokelewa na walinzi getini ambao mara baada ya kumsikiliza shida yake, walimjibu kwa ufupi ya kwamba, ametapeliwa, jengo hilo halina ofisi ya asasi hiyo japo walikiri kuwepo kwa watu wengi wanaofika eneo hilo kwa shida hiyo.
Mwandishi wa habari hizi alitaka kujua kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ina taarifa yoyote kuhusu utapeli huo unaofanywa na asasi hiyo kwa njia ya mtandao, hatua zipi zimechukuliwa dhidi ya matapeli hao, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TCRA Joseph Mungi alisema, taarifa hizo wanazo, tayari uchunguzi wa polisi, kitengo kinachoshughulikia makosa kwa njia ya mtandao (Siber Crime), umeanza.
Hata hivyo Kamishina wa kitengo hicho kinachoshughulika na makosa kwa njia ya mtandao aliyejuliakan kwa jina la Andrew, hakuweza kupatikana Jumamosi kuzungumzia suala.
Kwa upande wake kiongozi wa Polisi Jamii, makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwakaluka alisema, amepokea malalamiko ya Makumila ambaye aliahidi kulishughulia suala hilo.
No comments:
Post a Comment