Monday, 22 July 2013

HII NDIYO NYARAKA NYETI YA CCM ILIYONASWA NA CHADEMA, MBOWE AIONESHA MKUTANONI



Chadema cha Demokdrasia na Maendeleo (Chadema) kimesisitiza kuwa kitasimamia azimio la kikao cha Kamati Kuu yake kuhusu kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na usalama na kuibua nyaraka ‘nyeti’ za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinazoweka hadharani mikakati ya CCM kufundisha vijana kukabiliana na wapinzani.

Pia kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuachia madaraka kama amechoka kuendelea kuwa kiongozi anayepaswa kusimamia misingi ya uongozi bora, ikiwamo kufuata haki za binadamu, sheria na demokrasia kwa ajili ya ustawi wa jamii ya Watanzania. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara, katika viwanja vya Mahakama ya Mwanzo, Nguzo Nane, mjini Shinyanga juzi.

Alisema ili kujilinda dhidi ya vitendo alivyodai wanafanyiwa na vijana wa Green Guards wanaotoka kikosi cha vijana wa CCM, Chadema itaendelea na mipango ya kuwapa vijana wake mafunzo ya ukakamavu.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mji huo na vitongoji vyake, Mbowe alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa chama hicho kupitia wanachama wa Umoja wa Vijana (UVCCM), kimekuwa kikitoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha kuwa moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kukabiliana na upinzani.

“Tunashambuliwa, watu wetu wanapigwa, wanateswa, wanatekwa na wengine kuuawa, kwa sababu tu wanataka mabadiliko na wanapenda Chadema,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Majuzi mlisikia Waziri Mkuu, Pinda anasema wamechoka...sasa tunasema, Pinda  kama umechoka ondoka upishe ofisi ya umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya watu kama umechoka. Maana kuchoka huko ni kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi siyo za kwenu hizo, ni za Watanzania.”

“Wananchi hapa mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM. Moja ni cheti cha kuhitimu mafunzo na nyingine hapa juu imeandikwa: ‘Sera za Msingi za CCM’. Sasa mi sitawasomea. Naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua kusoma, awasomee mjue tunaposema CCM wamekuwa na kikundi kinachoshambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua Watanzania wenzao eti tu kwa sababu wanaunga mkono Chadema, huwa tunamaanisha nini.”

Mmoja wa wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni sehemu ya shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki (mikoa ya  Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa lililoandikwa: “Sera za Msingi za CCM” na kusoma sehemu inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho.

Kifungu cha 9.1 kinachozungumzia UVCCM kinasomeka kuwa:

‘Umoja wa vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika itikadi, ukakamavu na mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya kutimiza wajibu wao wakiwa walinzi wa wa chama, viongozi na wagombea wa CCM.’

‘Utaratibu wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa dhati. Chama kiwe na mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakaofaa kuwapatia vijana mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya uchaguzi/uraia.’ 

‘Mafunzo ya makambi ya vijana, mbali ya kujifunza nyimbo za hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani,’ inasomeka sehemu ya kitabu hicho cha CCM. Mbowe pia alimwomba mtu huyo asome cheti cha mmoja wa wahitimu wa kile alichodai ni mafunzo ya makambi ya vijana wa CCM.

Cheti hicho kinaonyesha mhitimu alianza mafunzo Juni 27, 2009 na kumaliza Julai 4, 2009, Wilaya ya Dodoma mjini, kimesainiwa na watu wawili; mmoja mwenye jina la Jumanne Kitundu, akiwa ni Katibu wa UVCCM, Dodoma Mjini na mwingine, ni Robert Mwinje, Mwenyekiti wa Umoja huo Wilaya ya Dodoma Mjini.

Pia cheti hicho kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa) alihitimu mafunzo ya kanuni ya UVCCM, wajibu wa vijana katika chama, ulinzi na usalama, ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana katika uchaguzi, rushwa, Ukimwi, historia ya Tanu na ASP pamoja na maadili.

Katika mkutano huo, Mbowe aliwataka Watanzania kuacha kugombana kwa sababu ya vyama, badala yake wasumbuliwe na waunganishwe pamoja na matatizo yanayowakabili sasa, ambayo alidai yanasababishwa na uongozi mbovu wa CCM.

Alisema Chadema inajiandaa kusambaza ushahidi ilionao wenye tuhuma nzito dhidi ya CCM kushindwa kufanya siasa na kuongoza nchi, badala yake imekuwa ikishambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua watu.

Ushahidi huo umewekwa kwenye kitabu kimoja ambacho kwa mujibu wa Mbowe, kitatolewa nakala nyingi, kinaonyesha matukio mbalimbali ya kisiasa ambayo wananchi wamepigwa, wameumizwa na wengine kuuawa katika shughuli za siasa, huku uchunguzi huru ukiwa haujawahi kufanyika kubaini wahusika wa matukio hayo na sheria kuchukua mkondo wake.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche, katika mkutano huo, aliifananisha kodi mpya ya kadi za simu kuwa ni zaidi ya iliyokuwa kodi ya kichwa ambayo ilifutwa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...