TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeahirisha tena uchaguzi wa madiwani kata nne za Arusha hadi Julai 14 kuruhusu kurejea utulivu baada ya mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema ulioathiri uchaguzi huo wiki iliyopita.
Bomu hilo lilirushwa Juni 15 na mtu asiyejulikana katikati ya mkutano
wa Chadema katika viwanja vya Soweto, mjini Arusha na kusababisha vifo
vya watu watatu na wengine kujeruhiwa na uchaguzi huo wa Juni 16
kulazimika kuahirishwa.
Baada ya tukio hilo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Arusha aliuahirisha
hadi Juni 30, lakini jana Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema
utafanyika Julai.
Kata zinazohusika ni Elerai, Kimandolu, Thani na Kaloleni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Jaji Lubuva alisema walipotangaza
kuwa uchaguzi ungefanyika Juni 30 waliamini kuwa hali ya utulivu na
amani ingekuwa imetengemaa.
“Lakini kwa bahati mbaya tumejiridhisha kuwa hali bado inahitaji
kuangaliwa kuhakikisha imerejea katika utulivu wake kikamilifu. “Hiyo
haimaanishi kuwa ni mbaya, isipokuwa tumeona bado tunahitaji muda wa
kama wiki mbili hivi kuona vumbi lililokuwa likitimka limetulia,” Jaji
Lubuva alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, wapiga kura hawapaswi kutekeleza haki yao
ya kupiga kura katika wasiwasi hivyo ni wajibu wa Tume kuhakikisha
unaondoka na wapiga kura wanatekeleza haki yao kwa amani.
“Tunataka watu wajihisi huru wakati wa kupiga kura, ndiyo maana
tumeahirisha uchaguzi wa kata hizo kwa mara nyingine. Wanapokuwa na
amani na uhuru wapiga kura wanaweza kuchagua wanayemtaka kwa utaratibu
mzuri, vinginevyo, shughuli yote ya kupiga kura inaweza kuharibika,”
alisema Lubuva.
Aidha, alitaka wagombea na vyama kutoendeleza kampeni kwa sababu
kuahirishwa kwa uchaguzi hakumaanishi kuwaongeza muda wa kujinadi au
kutafuta wapiga kura wa kuwaunga mkono.
“Muda wa kupiga kura haujabadilika. Vituo vya kupigia kura
havijabadilika na vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa 10
jioni.
Waliokuwa katika mstari ndio watakaopiga kura na watakaofika
vituoni baada ya muda huo kwisha hawataruhusiwa kupiga kura ili kutoa
nafasi ya kura kuhesabiwa,” alisema.
Jaji Lubuva alisema matokeo ya uchaguzi huo mdogo yatatangazwa mapema
na taratibu za uchaguzi zitazingatiwa ili kutoa haki kwa wapiga kura na
wanaopigiwa kura.
Inadaiwa bomu hilo lililokuwa kwenye mfuko wa plastiki, lilirushwa na
mtu asiyejulikana. Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Amir Ally
(7), Judith Moshi na Amir Ally.
No comments:
Post a Comment