ALIYEKUWA Meneja wa Kampuni ya Malawi Cargo tawi la Mbeya Evason Mwale(49) raia wa nchi jirani ya Malawi, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbeya akituhumiwa kujihusisha na Rushwa ya Ngono.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Basilius Namkambe akisoma Mashtaka ya mtuhumiwa huyo mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Gilbert Ndeuluo alisema Mtuhumiwa anashtakiwa kwa makosa mawili ambayo ni Rushwa ya Ngono kinyume cha kifungu cha 25 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007.
Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo April 11, Mwaka huu katika Hoteli moja iliyopo Iyunga Jijini Mbeya ambapo alikamatwa akitaka kujihusisha na rushwa ya Ngono na Mke wa Mfanyakazi wake.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Ndeoruo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 1, Mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ambapo pia alisema Dhamana iko wazi kwa Mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili wenye hati za mali isiyohamishika yenye thamani ya Shilingi Milioni 10, Barua zinazotambuliwa na mamlaka, ambapo pia mtuhumiwa anatakiwa kuacha hati zake za kusafiria na kutoruhusiwa kutoka nje ya Jiji la Mbeya bila ruhusa ya mahakama.
Awali ilidaiwa kuwa Meneja huyo alitaka kujihusisha na Rushwa na Mke wa Mfanyakazi wake wa nyumbani ambaye alimfukuza kazi na baadaye alimtumia Mkewe ili amrudishe kazini baada ya kufanya naye mapenzi.
No comments:
Post a Comment