Hatua hiyo ilitokana na mapendekezo ya Tamongsco yakitaka Serikali
ipeleke wanafunzi kwao na kuwalipia ada, kupitia mfumo wa ushirikiano wa
Sekta Binafsi na ya Umma (PPP).
Katika mapendekezo yao, walitaka Serikali ipunguze msongamano wa
wanafunzi waliozidi katika shule zake, kwa kuwapeleka katika shule
binafsi. Akijibu hoja hizo, Rais Kikwete, aliyealikwa kuhudhuria,
alisema wazo hilo ni zuri lakini lina changamoto.
“Nimesikiliza kwa makini sana hoja yenu ya kutaka kushirikiana na
Serikali kuondokana na msongamano wa wanafunzi katika baadhi ya shule
zake. “Natambua kwamba wakati Serikali inahangaika kupunguza msongamano
kwenye shule zake, baadhi ya shule zenu zina madarasa yaliyo wazi na
zingependa kuletewa wanafunzi na Serikali,” alisema Rais.
Rais alifafanua kwamba pamoja na uzuri wa wazo hilo, suala hilo lina
changamoto zake kutokana na ukweli kwamba gharama katika shule hizo ni
kubwa, hivyo wazazi au Serikali hawataweza kumudu. Ombi la JK Kutokana
na hali hiyo, Rais Kikwete katika mkutano huo wenye kaulimbiu ya
‘Changamoto na fursa zilizopo katika ushirikiano baina ya sekta ya umma
na isiyo ya umma katika utoaji wa elimu bora’, alitaka walimu hao
kujadili tatizo hilo la ada kubwa.
“Nina ombi moja kwenu ambalo napenda mlijadili kwenye mkutano wenu. Ombi
lenyewe si geni, linahusu ada kubwa zinazotozwa na shule au vyuo vyenu.
Wapo wananchi wengi ambao wangependa sana kunufaika na elimu nzuri
mnayoitoa, lakini wanashindwa kutokana na ada inayotozwa kuwa kubwa.
“Sisemi ada zenu zifanane na za shule za Serikali, lakini baadhi ya
shule na vyuo vyenu vinalalamikiwa na wananchi kwa kutoza ada kubwa na
kwamba hazitabiriki kwani hupandishwa wakati wowote,” alisema Rais
Kikwete.
Tathmini Pamoja na ombi hilo kwa Tamongsco, Rais Kikwete alisema
Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeliona hilo na
imeamua kulifanyia kazi. Alisema tathmini ya gharama halisi za
uendeshaji kwa mwanafunzi mmoja, itafanywa ili kutoa ushauri stahiki kwa
wamiliki wote wa shule au vyuo kuhusu kiwango cha ada.
Alirejea kauli yake, kwamba elimu ni huduma muhimu na haki kwa mtoto na
si vema kugeuzwa kuwa biashara ya kuleta faida kubwa. Alisema hadi sasa
uthamini kwa vyuo vya elimu ya juu umeshafanyika na mapendekezo ya
gharama halisi yameandaliwa.
Rais alisema tayari hatua za kumpata mtaalamu elekezi zimefanyika, kwa
ajili ya kutathmini gharama za uendeshaji kwa shule za sekondari. Hata
hivyo, aliwahakikishia Tamongsco kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono
na kushirikiana nao, ili kuwawezesha vijana wengi zaidi wa kitanzania
kupata elimu.
“Tutaendelea kupokea na kufanyia kazi ushauri wenu ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu.”
Sera ya Elimu Wakati huo huo, Serikali imesema Sera mpya ya Elimu
inatarajia kuanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu ambapo pia mitaala ya
elimu itapitiwa upya, ili kwenda sambamba na sera hiyo.
Rais Kikwete alisema mchakato wa kutunga sera hiyo mpya ya elimu baada
ya ile ya mwaka 1995, umefikia hatua za mwisho na kinachosubiriwa sasa
ni maoni ya wabunge ili sera ikamilishwe.
“Naamini kabla ya mwisho wa mwaka huu, sera itakuwa tayari kutumika,
tunaamini kuwa sera hiyo mpya italeta mabadiliko katika uendeshaji wa
mifumo yetu ya elimu nchini, na kutoa majibu kwa maswali mengi,”
alisema.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, nafasi ya sekta binafsi katika kuchangia
maendeleo ya elimu nchini itafafanuliwa kwa upana na kina zaidi.
Alifafanua, kwamba mitaala mipya itakayotokana na sera hiyo, itakwenda
sambamba na hali ya sasa na mahitaji ya maendeleo nchini na duniani,
huku akiwahakikishia kuwepo kwa ushirikishaji wa wadau, wakiwamo wa
sekta binafsi katika suala hilo. Idara ya Elimu Kuhusu Idara ya Ukaguzi
wa Elimu, Rais alisema itapewa kipaumbele na Serikali inatambua kuwa
hali ilivyo sasa hairidhishi.
“Serikali imeanza na inaendelea kuchukua hatua thabiti kuimarisha
ukaguzi wa shule na vyuo nchini, miongoni mwa mambo yanayofikiriwa
kufanywa ni kubadili Idara ya Ukaguzi kuwa taasisi inayojitegemea na
kuiwezesha kwa rasilimaliwatu, vitendea kazi na fedha,” alisema
Alisema anaamini kwa njia hiyo, wataimarisha utendaji wa ukaguzi na
matokeo yake yataonekana kwa muda mfupi na kuwakumbusha kuwa mkaguzi wa
kwanza wa shule ni Mkuu wa Shule.
No comments:
Post a Comment