Friday, 3 May 2013
HOTUBA YA MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA (MB), WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
Hotuba ya Mhe. Dkt. Shukuru J. Kawambwa (MB), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa Tamongsco uliofanyika Aprili 30, 2013 katika ukumbi wa Benjamin W. Mkapa, soko matola, Mbeya.
Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Ndugu Mahmoud Mringo,
Rais wa shirikisho la shule zisizo za Serikali za Malawi (ISAMA), Bw. Joseph Patel,
Mwenyekiti wa TAMONGSCO, kanda ya nyanda za juu na mwenyeji wa Mkutano, Fr. Innocent Sanga,
Ndugu Makamu Mwenyekiti wa TAMONGSCO,
Ndugu Katibu Mkuu wa TAMONGSCO,
Ndugu Naibu katibu Mkuu wa TAMONGSCO,
Ndugu Mhazini wa TAMONGSCO,
Ndugu Viongozi wa kanda 11 za TAMONGSCO,
Ndugu washiriki wa Mkutano: Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali,
Ndugu wawezeshaji - Bank of Africa,
Ndugu wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kushiriki katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) hii leo. Napenda kutumia fursa hii pia kukushukuru kwa dhati wewe Mheshimiwa Rais kwa kukubali kutenga muda wako adhimu ili kushiriki nasi na kutufungulia Mkutano huu muhimu katika Sekta ya Elimu, ambao kauli mbiu yake ni “Changamoto na fursa zilizopo katika ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Isiyo ya Umma katika utoaji wa elimu bora”.
Mheshimiwa Rais,
Wajibu wangu leo si kutoa hotuba katika Mkutano huu, lakini kabla ya kukukaribisha uzungumze na wadau wetu hawa muhimu katika utoaji wa elimu, nakuomba Mheshimiwa Rais, uniruhusu nitumie fursa hii kuelezea machache kuhusu ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Rais,
Wizara yangu imeendelea kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, ambayo inasisitiza ushirikishaji wa sekta binafsi katika kutoa elimu kwa kuanzisha na kuendesha shule na taasisi zingine za elimu hapa nchini. Tangu kuanza utekelezaji wa Sera hii, watu binafsi na mashirika mbalimbali yakiwemo ya dini, wameanzisha na kuendesha shule za msingi, za sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu. Mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu ni mkubwa na unaendelea kuongezeka kila mwaka kwa kadri wanavyoendelea kujenga na kufungua shule na Vyuo vipya. Wajibu wa Wizara yangu ni kuzikagua asasi hizo na kuzisajili kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Rais,
Wanufaikaji wa elimu inayotolewa na Sekta binafsi wamekuwa wakiongezeka sana kila mwaka. Kwa mfano, hadi Juni,2012 kati ya Wanafunzi 1,034,729 wa Shule za Awali, wanafunzi 49,669 wako katika shule zisizo za Serikali na kati ya Wanafunzi 8,247,164 wa shule za msingi, wanafunzi 227,424 wako katika shule zisizo za serikali. Katika shule za Sekondari zenye jumla ya Wanafunzi 1,884,272, kati yao wanafunzi 281,520 wanasoma katika shule za sekondari zisizo za serikali. Aidha, vipo Vyuo vya Ualimu 34 ngazi ya Cheti na Stashahada vya Serikali vyenye jumla ya Wanachuo 26, 626,ambapo pia vipo vyuo ualimu 88 vyenye jumla ya wanachuo 16,632 visivyo vya Serikali. Huu ni mchango mkubwa sana unaotolewa na Sekta hii hapa nchini.
Mheshimiwa Rais,
Kutokana na kukua kwa Sekta binafsi katika kutoa huduma ya elimu, ni dhahiri changamoto hazikosi kuwepo na ndiyo maana ya Mkutano huu wa leo ambao utajadili namna ya kuzikabili changamoto na pia kuishauri Serikali. Lakini nikiri kuwa, viongozi hawa wa TAMONGSCO ni shupavu na wako imara, wenye dhamira madhubuti ya kufikia malengo yao. Nayasema haya kwa sababu, tumeshakutana nao katika vikao mbali mbali, lengo likiwa ni kubadilishana mawazo na serikali, namna tunavyoweza kuzikabili Changamoto zilizopo kwa pande zote mbili na pia kuimarisha Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta hii binafsi katika utoaji wa elimu bora nchini.
Mheshimiwa Rais,
Baadhi ya mambo yaliyoelezwa katika risala ni yale tuliyokuwa tunaendelea kujadiliana. Baadhi yake tumeshajipanga kuyatafutia ufumbuzi. Kwa sasa Wizara yangu ipo katika kukamilisha utafiti wa gharama halisi ya kusomesha mwanafunzi (unit cost) kwa Vyuo vya Elimu ya Juu. Matokeo ya utafiti huu, yatatupa mwongozo wa namna nzuri na vigezo vya kufanya utafiti mwingine wa gharama halisi kwa mwanafunzi katika elimu ya msingi, sekondari na vyuo. Lengo la kufanya utafiti wa gharama hizo ni kuwa na vigezo vya kutumia katika kupanga ada ili kuwa na uwiano unaofaa kwa wenye shule na walipaji wa ada hizo.
Aidha, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wamiliki na Mameneja wa shule zisizo za Serikali katika kuendelea kuyatafutia ufumbuzi wa masuala mbambali yanayo ikabili sekta ya elimu kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Rais,
Baada ya kusema hayo machache naomba sasa kwa heshima nikukaribishe Mheshimiwa Rais uongee na wajumbe wa mkutano huu na kisha utufungulie rasmi Mkutano Mkuu Maalum wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyokuw vya Serikali Tanzania.
Mheshimiwa Rais, Karibu sana.
Labels:
habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment