Thursday, 4 July 2013

MICHELLE OBAMA:ACHENI KUFUATILIA MAVAZI YANGU

Michelle Obama na Laura Bush walikuwa kivutio jana kwenye Mkutano wa wake wa marais wa Afrika unaoendelea Dar es Salaam, pale walipoongelea kwa mzaha jinsi vyombo vya habari vinavyoshupalia kuandika kuhusu staili za nywele na  mavazi ya wake wa marais, huku vikiacha masuala ya msingi.

Mkutano huo uliofunguliwa jana na Rais Jakaya Kikwete, ni maalumu kwa ajili ya kusaidia wanawake wajasiriamali wa



 
Afrika, unatarajiwa kumalizika leo.
Wakizungumza kwenye mjadala ulioongozwa na Mwandishi wa Habari wa Marerkani, Cokie Roberts,  Michelle, ambaye ni mke wa Rais wa Marekani, Barack Obama, alisema alifurahia kupata nafasi ya kufanya majadiliano na Laura, ambaye ni mke wa Rais wa zamani wa Marekani.
“Ninampenda mwanamke huyu,” alisema Michelle kwa utani kama vile hamfahamu.  
“Sishangai sana maana tuko klabu moja nadhani,”  alijibu Laura kwa utani akiwa na maana kuwa,  wao wote wana uzoefu wa kuwa wake wa marais.
“Unajua tunaishi maisha ya shida, maana wenzetu wa habari wanaangalia zaidi staili za mavazi na nywele zetu badala ya kuangalia mambo ya msingi,” alisema Michelle.
 Alisema mwanzoni mwa mwaka huu, alibadili staili ya nywele lakini alishangaa jinsi suala hilo lilivyokuzwa na vyombo vya habari.
“Watu wanapaswa kuelewa, wake za marais nao hufanya mambo mazuri ya jamii na kazi yao siyo kubadili staili za nywele na mavazi tu,” alisema Michelle, ambaye anasifiwa na majarida mbalimbali ya Marekani na Ulaya kwa mitindo yake ya mavazi na nywele.
“Nadhani ndugu zetu wanahabari watabadilika,” alitania Laura wakati wa mjadala huo.

Cherie Blair
Naye Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, Cherie, jana alitangaza mpango wa kuwasaidia wanawake wa Afrika kufanya biashara kwa kutumia mawasiliano ya simu.
Mpango huo unasimamiwa na Taasisi ya Cherie Blair Foundation kwa kushirikiana na Kampuni ya ExxonMobil.
Akitangaza mpango huo kwenye mkutano wa wake za marais wa Afrika, Cherie alisema watatoa mafunzo ili kufanikisha mkakati huo.
Cherie, ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, alisema  wameanza utekelezaji wa mpango huo nchini Tunisia.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...