Saturday 8 June 2013

OOH! ALBERT MANGWEHA KWAHERI MFALME

Waandishi Wetu Dar na Morogoro
KWAHERI mfalme wa freestyle! Ndivyo walivyokuwa wakisema mashabiki wa aliyekuwa mkali wa Hip Hop Bongo, marehemu Albert Kenneth Mangweha ‘Ngwea’ wakati wakiuaga mwili wake, tayari kwa safari ya kaburini.
Mwili wa marehemu Albert Kenneth Mangweha ‘Ngwea’.
Juzi (Jumatano) Ngwea aliagwa na maelfu ya watu katika Viwanja vya Leaders Kinondoni, jijini Dar na kusafirishwa kuelekea Morogoro ambako nako uliagwa tena kabla ya kupumzishwa katika Makaburi ya Kihonda.
Timu ya waandishi wa Global Publishers, Richard Bukos, Issa Mnally, Denis Mtima, Chande Abadallah, Imelda Mtema, Joan Lema, Mwaija Salum, Gladness Mallya, Musa Mateja na Dustan Shekidele wanakuletea yote yaliyojiri ambapo walikuwa wakiwasiliana na mkuu wao, Sifael Paul akiwa Makao Makuu, Bamaga-Mwenge, Dar.
Mwili wa Mangweha ukiwasili Viwanja vya Leaders.
HOFU YA KUTEKWA MWILI WA NGWEA YATAWALA MUHIMBILI
Mkuu akiwa ofisini anaanza kumtwangia Bukos aliyekuwa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Saa 1:36 asubuhi
Bukos: Mkuu nakupata vizuri, hivi tunavyoongea nipo mochwari hapa Muhimbili.
Makao Makuu: Nini kinaendelea hapo?
Bukos: Mkuu mwili wa Ngwea ndiyo unatoka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti lakini ulinzi ni mkali sana.
Makao Makuu: Vipi kuna mastaa gani hapo?
Bukos: Nawaona wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya akiwemo Mchizi Mox lakini chakushangaza wasanii wenyewe wanaonekana wamekuja kuuchukua mwili wa mwenzao huku wakiwa chakari.
Makao Makuu: Duh! Wasije wakaliangusha jeneza lenye mwili wa marehemu…nini kinaendelea?
Bukos: Mkuu sasa msafara ndiyo unatoka hapa mochwari ukiongozwa na gari la polisi limeandikwa OCS Buguruni, likifuatiwa na gari lililobeba mwili wa marehemu na mengine ya waombolezaji.
Makao Makuu: Enhe, mbona nasikia zogo?
Bukos: Mkuu kweli askari wa Muhimbili noma yaani licha ya msafara huu kuongozwa na gari la polisi lakini askari wa geti la kutokea ‘wamedinda’ hapa wanataka kibali cha kutolea mwili vinginevyo kama hakieleweki mwili hautoki.
Makao Makuu: Sasa inakuwaje?
Bukos: Hawa askari wa getini wamegoma kabisa wamesema hapa bila kibali, bora huo mwili urudishwe huko mochwari hata kama msafara unaongozwa na gari la polisi.
Makao Makuu: Kwa hiyo?
Bukos: Msafara umesimama hapa getini, namuona baba mdogo wa marehemu Ngwea, Mzee David Mangweha ameshuka anawaonesha kibali, kumbe alikuwa nacho alihifadhi kibindoni duh! Leo hapa sijui ingekuwaje, msafara unaendelea sasa kuelekea Viwanja vya Leaders Club.
Makao Makuu: Oke Bukos, ngoja niwasiliane na Imelda, yeye tayari yuko Leaders Club.
 
Saa 3:23 asubuhi
DIAMOND ‘AHARIBU’ MSIBA
Makao Makuu: Imelda natumai unanipata vizuri, hebu nijuze kinachoendelea hapo Leaders Club.
Imelda: Ka’ Sifael kwa upande wangu huku Kusini Mashariki mwa uwanja huu naona watu wanatawanyika lakini sijajua wanakimbilia nini maana utaratibu wote wa kuusubiri mwili umevurugika.
Makao Makuu: Hebu fuatilia haraka uniambie.
Imelda: Ka’ Sifael kumbe lile kundi lilikuwa linamkimbilia Diamond (Nasibu Abdul) yaani kundi limemzonga mpaka usalama wake sasa unaelekea kuwa shakani.
Makao Makuu: Dah! Hao watu wana vituko sana, yaani wameacha msiba wanamkimbilia Diamond?
Imelda: Ka’ Sifael namuona OCD wa Wilaya ya Kinondoni, Afande Mutafungwa anawaongoza vijana wake kumuokoa Diamond maana yuko  katika hali mbaya.
Makao Makuu: Duh! Sawa Imelda hebu ngoja niwasiliane na Mnally.

Saa 5:12 asubuhi
LINEX, H. BABA WANUSURIKA KUFANYIWA KITU MBAYA
Makao Makuu: Haloo… haloo … Mnally unanipata vizuri?
Mnally: Nakupata Mkuu wangu.
Makao Makuu: Haraka nieleze kinachoendelea hapo ulipo!
Mnally: Mkuu mwili umeshawasili hapa Leaders Club na shughuli za kuaga zinaendelea.
Makao Makuu: Vipi kuna kituko gani umekinasa hapo hadi muda huu, si unawajua hawa mastaa wetu hawakaukiwi vimbwanga?
Mnally: Mkuu nimepata taarifa kuwa Linex na H. Baba wamenusurika kuporwa mali zao na vibaka.
Makao Makuu: Mnally fuatilia kwa ukaribu halafu unijulishe juu ya hizo taarifa.
Mnally: Sawa Mkuu lakini nimewasiliana kwa SMS na H. Baba ameniambia kuwa wameokolewa na mabaunsa, wapo salama kabisa.
Makao Makuu: Safi sana Mnally endelea kupiga kazi mimi ngoja nimcheki Glad naona anabipu.
Mnally: Sawa Mkuu.

Saa 5: 23 asubuhi
KIBAKA NUSURA ACHOMWE MOTO MSIBANI
Makao Makuu: Haya, niambie kwa upande wako nini kinaendelea hapo ulipo Glad?
Gladness: Bosi hapa watu wanasukumana tu, wanagombea kwenda kuuaga mwili wa mpendwa wao sasa imekuwa kama fujo. “Huyooo piga ua choriii chori kapetooo…choma moto mijizi hiyooo”
Makao Makuu: Glad, hizo kelele za nini tena?
Gladness: Yaani bosi kuna kibaka kakwapua mkoba wa mdosi f’lani ndiyo huyo mdosi na waombolezaji wanamkimbiza lakini kibaka mwenyewe ameshajichanganya kwenye huu umati, sijui kama watampata.
Makao Makuu: Sawa Glad piga kazi ngoja niwasiliane na Denis.
Gladness: Sawa Mkuu.

Saa 6:28 mchana
BONGO MUVI WAWAKIMBIA MASHABIKI WAO
Denis: Haloo! Mkuu simu yako mbona iko bize sana?
Makao Makuu: Hiyo siyo kazi yako kujua, niambie nini kinaendelea hapo ulipo?
Denis: Mkuu nawaona wasanii wa Bongo Muvi kama tisa hivi, wakiongozwa na Ray na JB. Lakini nashangaa wote wanajisweka kwenye gari moja, nahisi wanalikwepa kundi la mashabiki ambalo limeanza kuwazonga.
Makao Makuu: Sawa Denis hakikisha unanitafutia matukio nyeti kwa maana wewe mastaa wengi hawakujui, ngoja niwasiliane na Chande.
Denis: Sawa Mkuu.

Saa 7:00 mchana
SAFARI YA NGWEA KUELEKEA MOROGORO YAANZA
Makao Makuu: Chande nieleze nini kinaendelea kwa upande wako?
Chande: Mkuu hivi tunavyoongea jeneza lenye mwili wa marehemu Ngwea limeshafungwa na limeshaingizwa kwenye gari tayari kwa safari ya Morogoro.
Makao Makuu: Vipi hali, ikoje hapo?
Chande: Hali ni ya simanzi, safari ndiyo hiyooo imeshaanza. Umati umejipanga pembeni na kupungia mikono gari lenye mwili. Mkuu inahuzunisha sana kwani mashabiki wake wanasema, ‘Kwaheri Mfalme wa Freestyle’.
Makao Makuu: Oke Chande, waambie wenzako waendelee na majukumu yao ya kila siku kwani Mateja tayari yupo njiani kuelekea Morogoro.
Chande: Sawa Mkuu.

Saa 10:20 jioni
MORO  WASUBIRIA MWILI BARABARANI
Makao Makuu: Mateja uko njiani na uliniambia karibu unaingia Morogoro, je, hali ikoje barabarani?
Mateja: Mkuu Barabara ya Moro-Dar imejaa watu, bodaboda kibao wanasubiri kuona mwili wa marehemu Ngwea. Nimeambiwa pia kwamba watu wengi walikuwa hawaamini hivyo wamejitokeza kwa wingi kutaka kuhahakisha kama kweli ni Ngwea.
Makao Makuu: Basi ukifika nyumbani utatujulisha nini kinaendelea. Ngoja niwasiliane na Shekidele yupo nyumbani kwa mama wa Ngwea atujulishe hali ikoje.
Saa 11: 30 jioni
KABURI LAJENGWA
Makao Makuu: Shekidele uko hapo nyumbani kwa mama Ngwea, je. Hali ikoje?
Shekidele: Watu ni wengi sana Mkuu. Huu ni msiba mkubwa sana kwa hapa Moro.
Makao Makuu: Kweli ni pigo kubwa kila kona ya nchi. Maandalizi ya mazishi yakoje?
Shekidele: Kinachosubiriwa ni mwili wa marehemu lakini kila kitu kipo sawa kwani hata kaburi tayari limeshachimbwa na sasa linajengewa.
Makao Makuu: Oke, endelea kupiga kazi na Mateja anakuja kukuongezea nguvu.
Shekidele: Oke Mkuu.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa safari ya mwisho ya Ngwea ambapo alitarajiwa kuzikwa jana.
Ngwea alifariki dunia usingizini wiki iliyopita katika kifo tata akiwa Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...