Clouds
Media jana walifungua mdomo kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miezi
mitano tangu Jay Dee alipokuwa akiwarushia makombora kwa madai kuwa
wameharibu soko la muziki wa Bongo Fleva sambamba na kuitangaza bendi ya
Skylight kwa ajili ya kuiangamiza Machozi Bendi.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam ambapo pia alikuwa akirushwa moja kwa moja
katika redio ya Clouds FM, Mutahaba alisema Jay Dee amekuwa akilalamikia
mambo mawili ambayo ni bendi ya Skylight na matangazo yake
yaliyoshindwa kurushwa hewani japo alilipia Sh 240,000.
Alisema
suala hilo walilimaliza baada ya kumueleza kuwa redio yao haiwezi
kukataa matangazo kwakuwa ndiyo wanayowafanya waendelee kuwa kinara
katika suala zima la kuiendesha Clouds FM.
“Nilimwambia
kamwe hatuwezi kukataa matangazo na kama kuna lolote limefanyika, basi
ni kwa bahati mbaya, ukizingatia kuwa tayari alishafanya kazi nyingi
pamoja na kupewa urahisi kwenye kazi zake kwa kupitia Clouds FM.
“Pamoja
na yote hayo, bado matusi na kejeli yaliendelea hasa katika mitandao ya
kijamii jambo lililotufanya tuamuwe sasa kujibu japo hapo kabla
tuliamua kubaki kimya kwa ajili ya kulinda hadhi ya kazi zetu,” alisema.
Kuhusu
shutuma za kuitangaza zaidi Skylight Bendi, Ruge alisema bendi hiyo si
mali ya Joseph Kusaga, Mkurugenzi wao wala yeye, kama madai hayo
yanavyotolewa bila kufanya utafiti, isipokuwa ni mali ya Sebastian
Ndege.
“Kama
kuna mvutano kati ya Machozi Bendi na Skylight basi ni wa kibiashara
maana wote wanalipa fedha za matangazo na kama chanzo ni Jay Dee kuporwa
wanamuziki wake, hilo si jambo geni kwenye muziki.
“Dada
yangu Asha Baraka asingekuwa makini angelia sana, maana kila bendi
inayoanzishwa au kuendeshwa lazima ichukuwe wanamuziki kutoka kwake,
ukizingatia kuwa ni jambo la kawaida hivyo tumuomba Jay Dee atumie
busara katika hili pamoja na kuumiza kichwa kupokea ushindani na
changamoto kama hizo za kuchukuliwa wanamuziki,” aliongeza Ruge.
Aidha,
Ruge alisema Clouds FM ni redio ya watu binafsi, hivyo si ina utaratibu
wake katika utendaji wa kazi, ikiwapo kuchagua nyimbo au kuacha kupiga
kama kuna mtu amekwenda kinyume, hasa wale wanaopita nje na kuanza
kuwatusi, kuwakejeli bila kukumbuka fadhira walizofanyiwa kabla ya kuwa
maarufu wao.
Pia
alisema Clouds FM ipo tayari kufanya majadiliano ya wazi na mtu yoyote
mwenye hisia tofauti juu yao, huku ikiwataka wasanii waongeze bidii
katika kazi zao ili wasimlaumu mtu wanapoanguka na kuwapisha wengine,
maana muziki unaonekana ni wa kupokezana vijiti.
Katika
siku za hivi karibuni katika vyombo vya habari hasa hasa kwenye
mitandao ya kijamii nchini kumekuwa na taarifa rasmi na zisizo rasmi
kutoka kwa Mwanamuziki Lady Jaydee alilalamikia Kituo chetu cha Clouds
FM na wakurugenzi wake Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga.
xxxxx
SPEECH YAKE HII HAPA
RUGE MUTAHABA
Kwa
mtazamo wangu, kila mwananchi ana haki ya kutoa maoni yake ingawa
kwenye nchi yetu ya Tanzania, tumezoea maoni hayo kutolewa kwa lugha ya
ustaraabu na staha.
Maoni
kuhusu nani wa kuja kwenye msiba wako au nyimbo za kupigwa kwenye msiba
wako ni haki ya kila mwananchi na hakuna atayeuingilia uamuzi huo.
Maoni pia ya redio gani mtu anaipenda au tv gani pia nayo ni utashi wa
mtu mwenyewe.
Uongozi
wa Clouds FM ulikuwa umefikia maamuzi ya kutojadili jambo hili kutokana
na kuamini kuwa ni tatizo binafsi la mtu na sio jambo lenye maslahi ya
Taifa hivyo kwa uhalali linahitaji majadiliano au mazungumzo binafsi.
Sura ambayo jambo hili limewekwa na kulifanya kama dharura ya kitaifa sio sahihi kabisa kutokana na kukosekana na hoja za kina za kuhitaji majibu na pili kukosekana kwa ujumla wa tija kwa tatizo hili kitaifa.
Bado
ninaamini linatakiwa kubaki kama tatizo la mtu binafsi ila inapofika
taarifa zikapotoshwa kwa nia ya kuwapa mtazamo tofauti wasikilizaji
wetu, Clouds FM inataka kuweka maslahi ya wasikilizaji, wabia wetu wa
biashara na watanzania wote mbele kwa kuwapa taarifa sahihi za jambo
hili.
Clouds
Media Group inapata lawama kubwa sana kutoka kwa watu wengi ambao
pamoja na kuunga mkono ukimya wetu wanajiuliza ni kwanini hatukufanya
jitihada za kumaliza tatizo hili bila kufika hatua iliyofikia sasa ya
matusi, kebehi na vitisho kutwa vinavyoelekezwa kwetu na pia vinaendelea
kuichafua tasnia ya muziki hasa hasa Bongo flava; ambayo imefika mahali
inaonekana kila changamoto inayomkabili msanii wa Bongo flava lazima
itatuliwe kwa njia za mabavu (matusi, vitisho na kuchafuana).
Lawama hizo sio za kweli
na naomba nirudi nyuma kidogo kwenye historia ya jambo hili. Tarehe 14
mwezi wa 12 mwaka 2012 kwenye tweeter account ya Jaydee, alipost
kifuatacho:
Nilichofanya ni kumpigia simu na kuzungumza nae. Akasema
sijaandika kwenye blog chochote, nikamwambia Jide mi nakuheshimu sana.
Nimekupigia kwasababu naamini kama kuna kitu chochote ni bora nisikie
kwako, nategemea na wewe pia utanipigia iwapo kuna jambo lolote lile. Tulikotoka
sisi hatutakiwi kuendeshwa na majungu na maneno ya mtaani.Hiyo ilikuwa
tarehe 14 mwezi December mwaka jana. Baada ya kama dk 10 hivi akanitumia
msg ( ambazo bahati nzuri nilizihifadhi) na kusema ni kweli alikuwa
ananizungumzia mimi kwa sababu kuna vitu kadhaa vinamsumbua na aliambiwa
mimi ndo nilihusika navyo.
La
kwanza, ‘nililipa matangazo ya shs laki mbili na 40 ila hayajachezwa na
wala sijarudishiwa hela yangu, nimeambiwa umekataza matangazo yangu ya
Nyumbani lounge yasipigwe’.
La pili, naruhusu watangazaji wangu wamtukane ikiwa ni pamoja na kupromote zaidi bendi ya Skylight.
Pamoja na kwamba yeye alinitumia message, mimi nilimpigia simu na kumpa ufafanuzi wa yote hayo niliyosema hapo juu.
Nikasema, Biashara
yetu sisi ni matangazo…..kwanini tukataze matangazo yako yasipigwe??
Labda bahati mbaya tu, jamaa anayebook matangazo alipitiwa kuyabook
kibinadamu ila Gadna si anakuja hapa kila wakati, kwann asimkumbushe
tu?? Tutayasogeza tu mbele hadi wiki inayofuata, kwanini niyakataze
wakati muda sio mrefu tumetoka kuleta biashara ya Repa bora wa bendi
hapo hapo Nyumbani lounge.
Niliendelea kujibu kuwa
sio kweli kabisa, siwezi kuruhusu jambo kama hilo na kama ni kweli
mtangazaji anamtukana anifahamishe ni nani na kwenye kipindi gani,
nitasikiliza kipindi na kama ni kweli nitamfukuza kazi ( Clouds ina
mitambo ya kuhifadhi matangazo yake yote kwa takribani miezi 9).
Hili
nilimjibu kwa kirefu kidogo ikiwemo kumwambia akaze buti maana Skylight
Band wanakuja juu nk nk. (Skylight Band ni bendi inayofanya vizuri sana
hapa mjini na ilipoanza ilichukua baadhi ya majina makubwa kutoka
Machozi Band).
Baada ya kumaliza mazungumzo tuliagana vizuri tu kwa miadi ya kukutana nikirudi maana nilikuwa safarini.
Kwahiyo
ukiniuliza Jaydee anacholalamika ni nini??? Jibu langu litakuwa ni hayo
mambo mawili maana hata nyie watanzania wenzangu mnaosoma mitandao ya
kijamii mtakubaliana na mimi kuwa amekuwa anashambulia personality zetu,
mimi na Mkurugenzi mwenzangu bila kuweka wazi hoja za msingi kuhusu
yale anayotutuhumu nayo. Nimejitahidi sana kuelewa tatizo
lake hasa ni nini na imekuwa inanipa shida kidogo?? Nimejitahidi sana
kufikiria ni mirija ipi ya biashara kwake imeingiliwa, nakosa majibu???
Clouds
FM ni ya watu na watu wanaweza kufanya makosa kweli na hata kusababisha
matangazo ya laki 2 na 40 yasirushwe, kwa hilo nilishazungumza na
Jaydee na kuomba radhi toka tarehe 14 December 2012. Clouds FM haina
ubia wowote ule na Skylight Band (ni bendi iliyoanzishwa na
Mtanzania)hivyo kuipromote ni katika misingi ile ile ya biashara kama
tunavyopromote bendi yeyote ile na vilevile Clouds FM pia haihusiki
kabisa na kutetereka kwa biashara ya chakula, vinywaji na bendi
inayofanyika Nyumbani lounge. Inashangaza hata kuhusishwa na biashara ya
Nyumbani lounge…!!!
Sina
ugomvi binafsi na Jaydee wala Gadna, na tarehe 12 February mwaka huu,
nilienda kuazima stools kwa ajili ya shooting kutoka kwenye sehemu yao
ya biashara ingawa yeye amekiri kuwa na ugomvi mkubwa na sisi binafsi na
Clouds kama chombo.
Nyimbo
yake iliyotoka ya Joto Hasira ilipokelewa vizuri sana kulinganisha na
nyimbo mbili zilizopita ‘Yeye’ na ‘Mimi ni mimi’ ambazo hazikufanya
vizuri pamoja na jitihada kubwa ya kuzipromote. Joto Hasira iliacha
kupigwa kutokana na shinikizo lake mwenyewe, ikiwa imeshachezwa mara 48
ndani ya wiki tatu toka imetoka wote tulipigwa na bumbuwazi na kujiuliza
ni kitu gani tumefanya kuambiwa hatupigi nyimbo na lawama nyingine.
Kama ofisi tukaona tukae kimya na kusubiri hatua inayofuata ukizingatia
tuliendea kupiga nyimbo na video hata baada ya maneno makali ya mwanzo.
Kauli haikubadilika, mbaya zaidi kauli za kebehi na kuchafuana
zikaongezeka hadi kufikia uamuzi wa sisi kama taasisi kuamua rasmi
kutopiga nyimbo zake hadi atakapofuta kauli zake na kuomba msamaha.
Kupiga
au kutopiga nyimbo kwa kituo cha redio ni jambo la kawaida na kwasababu
ni chombo binafsi ni muhimu kwa watu kama Jaydee na wasanii wengine (na
hata wananchi wa kawaida) kuelewa kuwa kila ofisi ina taratibu zake na
iwapo utatokea ukiukaji wa taratibu hizo, policy ndo zinaongoza maamuzi. Hebu
tujiulize, mbona sio mjadala wa Taifa msanii Diamond hapigwi karibu
miezi sita sasa kwenye station ya Magic FM, Ray C na Ali Kiba kwa karibu
mwaka mzima walikuwa nyimbo zao na video hazipigwi na East Africa hadi
walipoomba msamaha, hadi Yanga kwa muda mrefu walikuwa hawatangazwi
habari zao kwenye chombo kimoja cha habari. Hayo ni mambo ya ofisi
binafsi na hakuna anayeweza kulaumu maamuzi hayo.
‘Management
reserves the right of admission’……nani hajaona kibao hiki kwenye hoteli
nyingi tu nchini, nani asiyefahamu kuwa kuna hoteli ambazo ukienda kama
mwanamke peke yako unakataliwa? Hizi ni taratibu na kila mahali
zipo…..hata nyumbani lounge ndo maana Sam Machozi ambaye yuko Skylight
Band zamani alikuwa mwanamuziki wa Machozi Band amepigwa marufuku pale
Nyumbani lounge na halalamiki maana ni sehemu binafsi na ina taratibu
zake. Ni tofauti na sehemu za wazi za umma kama Mnazi mmoja au kituo cha
basi cha Magomeni.
Clouds
Media Group inafuata taratibu zote za nchi na za kimkoa ila na yenyewe
pia inaweka taratibu zake za uendeshaji. Sasa isifike mahali Clouds
inapoweka taratibu zake hizo na kuzitekeleza inaonekana inafanya makosa.
Yaani hata tarehe za kufanya show nchi hii tunatakiwa kupeleka maombi sehemu ili watu zaidi ya mmoja wasifanye show kweli??? Kwanini
tunachanganya ushindani na fitina…..acha ziwepo bendi 10
zinazoshindana, kuanzishwa kwa bendi nyingine kusiangaliwe kama fitna. Na hata mtu akianzisha bendi kwa kuchukua wanamuziki kutoka kwenye bendi nyingine, si ndio dhana ya ushindani???
Kama
ni kulalamika kuanzishwa kwa bendi nyingine au kuchukuliwa wanamuziki,
Dadaangu Asha Baraka si angeshafanya maandamano nchi nzima. Ila wote
tunatambua kuwa ni jasiri ndo maana anatulia na kuanza upya.
Mbona watu hawalalamiki baa zinapofunguliwa 10 mtaa mmoja, au saloon za nywele, moja jirani na nyingine. Ni lazima tukubali na tuzoea ushindani.
Pamoja na ushindani kingine ninachoomba kuwasihi watanzania wenzangu hasa hasa wasanii wetu zaidi
ni kuwa kila mtu na kila kitu kina ‘shelf life’. Watu wa zamani naamini
wanamkumbuka Power Mabula….alikuwa anatisha sana wakati ule. Au nani
anaweza kusahau umaarufu wa Mzee Nobert Chenga na Kundi la Muungano
cultural troupe au labda huko ni nyuma sana; nani anamkumbuka Kanda
Bongo Man, alicharge laki moja enzi hizooo….au labda hapa katikati
umaarufu wa Muumini, Mr Nice au mtu kama Saida Karoli (alijaza Stadium).
Wote hao walikuwa maarufu sana. Sasa wasanii hawa na wengine wanaokuja
wasipojiandaa kuelewa kuwa kila kitu kina muda wake, tutakuwa na taifa
la vijana ambao asubuhi mpaka jioni badala ya kuhangaikia fursa nyingi
zilizopo wataishia kutafuta mtu wa kumlaumu.
Ni
lazima Edibily Lunyamila atarithiwa sehemu yake na kina Mrisho Ngassa
ambaye naye muda utapita ni lazima atawaachia kina Simon Msuva. Wapo
watu kama kina Dully Sykes walioanza kujiandaa kwa kuwaachia kina
Diamond na wao kufungua studio na kuwa maproducer. Suala la kupokezana
vijiti halikwepeki kuanzia makazini, mpirani na hata kwenye sanaa. Cha
kufanya ni kujiandaa kwa maisha yako baada ya kugawa kijiti chako.
Taarifa
za kutaka kuua muziki wa Bongo flava kwa makusudi zinashangaza, ili
iweje sasa??? Clouds inategemea matangazo ya biashara kama asilimia 95
ya mrija wa mapato na muziki tunaopiga redioni ni sehemu ya maudhui
kwahiyo hakuna namna yeyote ile tutataka muziki huo upotee. Tunafanya
juhudi zote hizi kwasababu tunahitaji nyimbo bora na wasanii bora ili
tuweze kuendelea kuwa kituo bora cha redio.
No comments:
Post a Comment