
Panya mzee akiwa mwenye nguvu baada ya kuwekewa damu changa
|
Siku
hizi kumekuwapo na usemi kuwa uzee mwisho Chalinze, jijini (Dar es
Salaam) kila mtu ‘baby’ (mtoto). Hii ikiashiria watu hawapendwi kuitwa
wazee ingawa umri wao ni mkubwa.
Wamekuwa
na kauli hiyo ili kulazimisha mazingira kwamba bado wana uwezo wa
kufanya yote kama wenye damu changa lakini katika uhalisia si kweli.
Utafiti
wa vyuo vya Harvard na California vya nchini Marekani vikishirikiana na
Cambridge nchini Uingereza, unajenga mazingira ya kuifanya ndoto ya
wenye mawazo ya kuukataa uzee kuwa kweli.
Watafiti
hao walichukua damu ya panya mchanga na kumuingizia kwa aliyezeeka.
Walichobaini ni kwamba panya yule mzee alichangamka na kurejewa na nguvu
za ujana.
Matokeo ya utafiti huo yanatoa mwanya kwa wanasayansi kukaa kitako na kutengeneza dawa ambayo mtu akitumia anaweza kutozeeka.
Kutozeeka
huko ni kuendelea kuwa na dalili za ujana kama vile kutokuwa na
makunyanzi usoni na viungo kuendelea kuwa na nguvu ya kutekeleza mambo
yote kama kawaida hata wenye umri wa zaidi ya miaka 70.
Utafiti ulivyofanyika
Timu
ya watafiti hao wiki hii walitangaza kuwa wamegundua namna ambayo
wanaweza kumfanya panya mzee kutokuwa na dalili zinazofanana na umri
huo.
Wanasema
kwenye utafiti huo kuwa mara baada ya kuchukua damu ya panya mchanga na
kumuingizia aliyezeeka ghafla alibadilika na kurejewa na nguvu
zilizomfanya achangamke na kutenda kama vile bado hajazeeka.
Walichobaini
ni kwamba ile damu ilienda kuchangamsha ubongo kiutendaji na kuwezesha
kuimarika kwa utendaji wa mwili kwa jumla.Kwa kawaida mambo yote
yanayotendeka mwilini huongozwa na ubongo kwa kuhamasisha homoni fulani
kulingana na jambo husika.
Wanasema kwenye damu ya panya mdogo kuna aina ya protini ijulikanayo kama GDF11, ambayo wanahisi ndiyo iliyochochea jambo hilo.
Wakasema wanachofanya ni kuchunguza kama hii protini ndiyo inayochochea ujana.
Mtaalamu wa Tanzania
Akizungumzia
juu ya utafiti huo, mtaalamu wa Afya ya Jamii katika Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii Dk Alex Mwita anasema hakuna haja ya watu kujipa
matumaini kutokana na ugunduzi huo kwa sababu hadi kupatikana dawa
itakayotumika kwa binadamu inaweza kuchukua miaka zaidi ya 10.
“Huu ni ugunduzi kwa panya. Hadi kufikia mafanikio kwa binadamu, ni utafiti utakaochukua miaka mingi,” anaonya Dk Mwita.
Alisema
zipo tafiti nyingi kuhusukile kinachosababisha uzee na kujaribu
kutafuta njia za kuuzuia lakini bado mafanikio hayajapatikana.
Nini kinasababisha uzee
Wataalamu wanasema kuwa ni jambo ambalo liko wazi kwamba uzee unapozidi, mwili hushindwa kujimudu na hatimaye kusababisha kifo.
Utafiti
uliosimamiwa na mtaalamu wa Elimu ya Viumbe katika Chuo Kikuu cha
Michigan nchini Marekani, Dk John Langmore ulibaini kuwa mtu anakufa kwa
umri kutokana na viungo vya mwili kushindwa kutekeleza kazi zake
kikamilifu.
Hali hiyo inachangiwa na kasi ya seli za mwili kuzaliana kupungua kwa kiwango kilichopindukia huku zinazokufa zikiwa nyingi.
Mfumo
huo uko hivi, mtoto anapozaliwa ukuaji wake ni wa kasi sana. Hii
inatokana na uwiano wa seli zinazokufa kuwa kidogo zaidi ukilinganisha
na zile zinazozalishwa.
Uwiano wa seli zinazokufa na zinazozalishwa hufikia mahali ukalingana. Ikifikia kiwango hicho mtu huwa hakui tena.
Uzee unaanza pale uwiano wa seli zinazokufa kuwa wa juu zaidi kuliko zile zinazozalishwa.
Hali hiyo huanza kuusababisha mwili kusinyaa na kusababisha mikunjo sehemu mbalimbali za mwili.
Kasi
ya seli zinazokufa ukilinganisha na zinazozaliwa huendelea kuongezeka
na hali hiyo huendelea kuongeza makunyanzi na hata baadhi ya viungo
kupoteza uwezo wake wa kawaida.
Kinachosababisha seli kutozaliana
Dk
Langmore na timu yake wanaamini kufa kwa seli ni jambo la kawaida
lakini sababu ya kasi ya kuzaliana kupungua kulingana na umri, ni jambo
muhimu pia.
Waliamini ufumbuzi huo ndiyo utakaowapa sababu ya mtu kuzeeka na pingine kutafuta namna ya kuzuia uzee.
Walibaini kuwa DNA ndani ya seli ndiyo inayohusika katika kuwezesha seli kuzaliana au kutozaliana.
Wakabaini kuwa ina kichocheo ambacho kinasababisha mazingira hayo ya seli kutozaliana hasa mtu anapofikia umri mkubwa.
Dk Mwita anasema kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanyika kuna kitu kinachojulikana kisayansi kama Telomere.
Anasema
Telomere inauhusiana na seli kudumu muda mrefu ikiwa na uwezo wa
kuzaliana au la. “Telomere ni kama kamba ya kufunga viatu. Inapomalizika
unakua mwisho wa seli kuendelea kuzaliana,” anasema Dk Mwita.
Anafafanua kuwa watu wanaokuwa na Telomere ndefu ndiyo wanaishi muda mrefu na wale wanaokuwa na fupi, maisha nayo yanapungua.
Mtafiti
mwingine wa Marekani, Dk Ronald Klatz anaonya wanasayansi kutojikita tu
katika kuchunguza sababu za uzee kwa kutumia jeni na mfumo wa seli za
mwili.
Akasema ipo haja pia kuchunguza mienendo ya mwili unavyoguswa na namna za ulaji, mazingira na misongo ya mawazo.
Akasema hali hizo kwa namna moja au nyingine zinachangia mwili kuchoka na hata kupunguza kiwango cha kawaida cha mtu kuishi.
Imeandikwa na Leon Bahati wa mwananchi kwa msaada wa mitandao
No comments:
Post a Comment