Thursday, 16 January 2014

HII NDIO NJIA BORA YA KUTIMIZA MALENGO YALIYOKWAMA MWAKA 2013 - 2


MUNGU ni mwema maishani mwangu, hakika namshukuru kwa kila kitu akitendacho kwangu. Ahsante baba.

 Ni mada ambayo hakika imegusa wengi. Nimekuwa nikipokea simu mfululizo kutoka kwa wasomaji wakipongeza na kutaka kujifunza mengi. Kuna tuliobadilishana nao mawazo, nashukuru kuona kuwa mada iliwagusa.
Ni kweli. Lazima kuwepo na nguvu au sababu inayokusukuma au kukushawishi kulifanya jambo hilo. Ni vyema kama utawekeza nguvu na akili yako yote, tena kwa asilimia zote juu ya jambo unalotaka kulitimiza.
Jifunze maarifa mengi juu ya jambo hilo. Chukua ujuzi kutoka kwa watu ambao wanafanya jambo hilo. Endelea kujifunza kutokwa kwao. Maisha ni kujifunza.
Hakuna ukomo wa kujifunza, ndiyo maana katika makala haya kila siku huwa nasisitiza watu kujifunza zaidi kadiri wawezavyo.
JIWEKEE UKOMO WA KUTIMIZA MALENGO HAYO:
Hapa namaanisha kuwa, ni lazima uweke muda wa ukomo wa lini utatakiwa kutimiza malengo yako. Kamwe usijiwekee malengo ambayo hayana muda maalumu wa kuyatimiza.
Mwanasaikolojia maarufu nchini Marekani, Willie Jollie katika kitabu chake cha It Only Takes A Minute to Change Your Life, aliandika: “A dream without deadline is just a wish.”
Hapo alimaanisha, ndoto au lengo lisilokuwa na muda wa lini litimie ni kama tamanio tu. Jipangie muda muafaka wa kutimiza malengo yako. Kufanya hivyo utaweza kujituma na kujitahidi kutimiza malengo hayo kwa kuangalia muda uliojipangia.
MUHIMU:
Maisha ni safari iliyojaa misukosuko mingi. Kuna miiba, milima, miinuko na kila aina ya maumivu. Inahitaji moyo wa ujasiri na uliodhamiria kuvuka adha zote hizo.
Hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati mbaya. Jiepushe na mambo ambayo hayana umuhimu. Fanya mambo ya maana. Jiwekee malengo thabiti na  nadhiri ya kuyatimiza kwa wakati.
Ukizingatia hayo, hakika Mungu hatakuacha katika mihangaiko yako.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...