Saturday, 18 January 2014

AIBU:WAZIRI AZOMEWA NA WANANCHI MBELE YA WAZIRI MKUU PINDA

*Wananchi wadai amewatelekeza muda mrefu
*Serikali yaahidi kuwasaka walioua raia
MBUNGE wa Kiteto (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedicti Ole Nangoro jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Nangoro, alizomewa na wananchi katika mji wa Kibaya wilayani Kiteto mkoani Manyara wakati Pinda na uongozi mzima wa mkoa huo walipofanya ziara ya siku moja kujionea uhalibifu mkubwa uliyofanywa wiki iliyopita kati ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Kimasai ambapo watu 10 walipoteza maisha. 

Baada ya zomeazomea kuzidi, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliamua kumuokoa Nangoro kwa kumchukua na kumpeleka kwenye gari lake kisha kuondoka eneo la tukio.

Hatua ya wananchi kumzomea Mbunge wao, imekuja baada ya madai kuwa kwa kipindi kirefu amekuwa haonekani jimboni kushughulikia kero zao.

Pia walimtuhumu kwamba kabla ya tukio la mauaji kutokea walimwita lakini hakutokea kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa na kazi maalumu mjini Dar es Salaam.

Mkutano wa jana, uliitishwa uongozi wa mkoa ili kutoa nafasi Pinda kutoa tamko juu ya mauaji na uharibifu mkubwa uliyotokea baada ya wakulima kupambana na wafugaji wa jamii ya Kimasai wiki iliyopita.

Mmoja wa wananchi hao, Zaina Hassani Chuma, alisema siku zote wamekuwa wakimwita mbunge huyo, lakini amekuwa mgumu kujitokeza kuwasikiliza

“Hatumhitaji mbunge kwa sasa, tulimwita kabla ya hata maafa hajatokea sasa anatafuta nini hapa baada ya kumwona Waziri Mkuu….hatukubali tunataka naye ahojiwe kuhusu maafa yaliyotokea na si vinginevyo”alisema. 

“Kama Waziri Mkuu, anataka kushughuhulikia tatizo hili kwa umakini aanze kuwakamata baadhi ya viongozi waliohusishwa na mgogoro huu, tena kwa bahati nzuri wanafahamika vizuri kwa kuchangisha fedha za wafugaji ili wawafukuze wakulima,”alisema.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa mkoa pamoja na Pinda, baada ya kusoma alama za nyakati hawakutoa nafasi kwa Nangora kutoa neon la pole kwa wapiga kura wake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...