Katibu Mkuu wa CCM ndg Abdulrahman Kinana amesema kinga ya Bunge isiwe sababu ya baadhi ya wabunge kutumia fursa hiyo kuchafua watu wasio na nafasi ya kujitetea ndani ya mhimili huo wa Dola.
Amehadharisha hayo alipozungumza
na waandishi wa habari mjini Dodoma juzi kukanusha tuhuma
zilizoelekezwa kwake binafsi na chama chake na Kambi ya Upinzani
Bungeni.
Tuhuma hizo zilihusu shehena ya pembe za ndovu iliyokamatwa Vietnam mwaka 2009 ambazo aliziita za kupika na za uongo."Tuhuma hizo hazina ukweli wowote, zina nia mbaya dhidi yangu na zimelenga kuniharibia taswira yangu na ya chama changu," alisema Kinana.
Alisema hahusiki vyovyote na
tuhuma hizo na kutuhumu Kambi ya Upinzani Bungeni kwa kushindwa kujadili
hoja za maana za maendeleo na badala yake kujihusisha na siasa za
kuchafua heshima za watu.
"Bado nina nguvu na sijayumba
kwa namna yoyote. Nina jukumu la kuilinda CCM na kutekeleza ahadi
tulizozitoa kwa wananchi kupitia ilani ya uchaguzi," alisisitiza na kushangaa suala hilo la tangu mwaka 2009, kujitokeza sasa.
"Jibu ni jepesi, lengo ni kumvunja moyo Katibu Mkuu wa CCM ambaye CHADEMA inamwona tishio kwao," alisema
Kinana na kusisitiza kuwa tuhuma dhidi yake hazina msingi na hata kambi
ya upinzani inatambua kuwa mamlaka zote za ulinzi na usalama za ndani
na nje zilimsafisha.
Kinana
alisema baada ya shehena hiyo kukamatwa, Mamlaka ya Kimataifa ya
Kudhibiti Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) na Polisi wa Kimataifa
(INTERPOL) walifuatilia na wakabaini kuwa hakuhusika.
Watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akiwataja
kuwa ni Eladius Colonerio (Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd), Gabriel
Balua (Meneja wa TEA Freight (T) Ltd) na Shaban Yabula (Mkurugenzi
Mtendaji wa Kigoma M.N. Enterprises (T) Ltd).
Wengine ni Erick Morand (Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika bandari ya Dar es Salaam) Issa Lweno, Norbert Kiwale na Abubakari Omar Hassan.
Kinana
alikana kumiliki meli yoyote na wala kujihusisha na usafirishaji wa
nyara hizo za Serikali. Katika mkutano huo, alimtuhumu Msigwa kuwa na
ajenda ya siri na kswamba aliamua kumtuhumu huku akijilinda kwa kinga za
Bunge na akijua kuwa kufanya hivyo ni kutumia vibaya kinga hiyo.
Kinana amesema anaamini chanzo cha kuchafuliwa kwake na wapinzani ni wadhifa wake.
Kinana alisema anaamini kuwa kama asingekuwa na wadhifa huo, asingesakamwa kwa tuhuma alizoziita za uzushi.
“Hivi
vitu havinisumbui. Hapa tatizo ni kuwa Katibu Mkuu wa CCM. ‘I am a
senior officer’ (Ofisa Mwandamizi) sasa katika chama changu kama
ningekuwa nimekaa nyumbani nafanya biashara zangu yasingetokea haya.
“Nataka
kuwaambia tu, waelewe kuwa hawawezi kunitoa katika ajenda yangu ya
msingi. Hii ni sawa na mwanajeshi anayekwenda kupigana vita na adui
halafu akawa na vikundi vidogo vinakushambulia kutoka kila upande
kukutoa katika lengo la msingi... ni lazima mtu ukomae na ili
ufanikiwe,” alisema Kinana.
Alisema
Msigwa alikuwa katika Kamati ya Ardhi na Maliasili ya Bunge tangu mwaka
2010 na ukweli wa mambo hayo anaujua... “Msigwa anajua kabisa nikiwa
kama ‘shipping agent’ (wakala wa meli), sihusiki na kujua kilichopo
ndani ya kontena. Wale wanaopaswa kujua ni meneja wa bandari, mamlaka ya
mapato, walinzi na wakala wa kupakia na kupakua mizigo, kwa kuwa wao
ndiyo wanafanya ukaguzi na kuweka seal (lakiri) …siyo kazi yetu,”
alisema.
Alipoulizwa
kwa nini hajachukua hatua za kisheria kama anaona amechafuliwa na kama
tuhuma hizo hazina ukweli? Kinana alijibu kuwa anajua kuna njia tatu za
kuchukua kuhusiana na tatizo hilo lakini bado anazifanyia kazi.
“Kwanza
unaweza kujieleza kwenye vyombo vya habari. Pia unaweza kukata rufaa
kwa Spika na kesi yako kusikilizwa lakini pia unaweza kwenda mahakamani.
Bado natafakari cha kufanya.”
---
Taarifa hi imenukuliwa kutoka kwenye magazeti ya HabariLeo na Mwananchi.
No comments:
Post a Comment