KWAKO,
Msanii wa filamu Bongo, Yobnesh Yusuph ‘Batuli’. Pole na mihangaiko ya
kujitafutia mkate wa kila siku. Naamini mishemishe zako zipo poa. Kwa
upande wangu mimi naendelea vizuri. Naamini sijawahi kukuandikia barua
hata mara moja, lakini nimeona ni vyema tuwasiliane kwa njia hii.
Lengo la kukuandikia barua hii ni kwa ajili ya kukuweka sawa, maana
naona kama njia unayoanza kupita siyo! Wenyewe wamekataza! Kwa muda
mrefu nimekuwa nikivutika na uigizaji wako, kama mdau wa sinema nchini
nilikuweka miongoni mwa wasanii wenye uwezo mkubwa sana wawapo nyuma ya
kamera.
Niliishia kuamini kuwa wewe ni msanii mkali, ambaye pengine siku zijazo
utakuwa nyota. Ni kweli, kwa sasa katika wasanii walio kwenye nafasi za
juu kabisa kwenye soko la filamu Bongo ni pamoja na wewe.
Najua jambo hili wengine hawapendi kukubaliana nalo hasa wasanii
wenzako, lakini nataka kukuhakikishia kuwa uko matawi ya juu kabisa.
Wakati fulani nilipata kufanya mahojiano na wewe nikiwa na jopo la
wahariri wenzangu. Hapo ndipo nilipogundua kuwa kumbe una uwezo
mwingine zaidi ya sanaa. Niligundua kuwa una uwezo mkubwa wa kufikiri
tofauti na matarajio ya wengi.
Kusema kwamba, ulitakiwa kucheza Filamu ya O’prah katika nafasi
iliyochukuliwa na msanii mwingine ili ushiriki kwenye vipande vya
kimahaba (love scenes) – ukakataa kilidhihirisha ukomavu wa uelewa
kichwani mwako!
Nilikusifu kwa hilo. Mpaka sasa naendelea kukusifia kwa hilo. Naamini
hata mashabiki wako wanakusifia kwa hilo maana ni jambo kubwa na la
maana sana.
Nikiwa nimekuweka kwenye nafasi hiyo, wiki iliyopita nikashangazwa na
jambo lililotokea kuhusu wewe. Nikajiuliza: Hivi ni Batuli huyuhuyu
ninayemjua au mwingine?
Batuli aliyekataa kucheza sinema yenye maudhui ya kimapenzi kwa hofu ya
kuharibu jina lake, leo hii anaweza kusema yupo tayari kucheza sinema za
aina hiyohiyo lakini nje ya nchi? Nikapigwa na butwaa. Batuli
amechanganyikiwa? Nikawaza.
Naamini hata kama ungekuwa ni wewe ungechanganyikiwa kama mimi. Batuli,
kwani hiyo sinema ukienda kucheza Nigeria na kuvaa mavazi ya hovyo,
haitasambazwa hapa Bongo na hatimaye wadau wakaiona?
Umesema tamaduni za nchi nyingine ni tofauti na zetu, ndiyo maana
unaweza kwenda kucheza, sawa lakini vipi kuhusu maadili yako kama
Mtanzania? Ukionekana kwenye sinema hata kama ni ya Marekani, umevaa
vivazi vya ajabu, itabadilisha jina lako la Yobnesh?
Sinema chafu hata ukicheza wapi, bado haiwezi kukubadilisha Batuli,
haiwezi kukuondolea Utanzania wako. Haiwezi kubadili chochote. Kila kitu
kitabaki katika uhalisi wake uleule!
Nadhani hukufikiri vizuri na kama mtazamo wako bado ni huo, nakuomba
sana tafakari tena – hauko sahihi. Jamii inakuamini sana, una uwezo
mkubwa wa kuwa staa zaidi ya ulivyo huku ukiendelea kuhifadhi maadili
yetu.
Chondechonde Batuli, fikiri tofauti.
Yuleyule,
Mkweli daima,
No comments:
Post a Comment