Wednesday, 8 May 2013

Balozi Seif Idd awaasa Watanzania kutohusisha tukio la mlipuko mkoani Arusha na masuala ya Kidini wala Kisiasa.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi akiangalia baadhi ya majeruhi wa mlipuko wa linalodhaniwa kuwa bomu uliotokea Jumapili iliyopita katika Kanisa Katoliki Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbali mbali Nchini mara baada ya kuwatembelea na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha baada ya kujeruhiwa katika mlipuko unaodhaniwa kuwa bomu katika Kanisa Katoliki la Arumeru Mkoani Arusha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na baadhi ya Viongozi wa Kanisa Katoliki Mkoani Arusha alipofika kuwafariji kufuatia mripuko wa unaodhaniwa bomu wakati  Viongozi hao pamoja na waumini  wao walipokuwa katika ibada ya Juma pili iliyopita.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nd. Yerembe Munasa Sabi akitoa Taarifa ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la Mlipuko unaodhaniwa kuwa Bomu mbele ya Viongozi wa Kanisa Katoliki na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kuwatembelea majeruhi wa mlipuko huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na  Balozi wa Papa Nchini Askofu  Mkuu Francisco Padilla Mjini Arusha.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Askofu Josephat Lebulu alipowatembelea kuwapa pole baada ya mlipuko wa Bomu Jumapili iliyopita.
Balozi Seif akisalimiana na Viongozi wa Dini ya Kikristo Mkoani Arusha wakati alipokwenda kuwapa pole kufuatia ajali ya bomu lililotokea Jumapili iliyopita katika Kanisa Katoliki la Arumeru Mkoani Arusha. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Watanzania kuacha dhana ya kulihusisha tukio la mlipuko unaodhaniwa kuwa ni bomu uliotokea katika Kanisa la Kikatoliki Wilayani Arumeru Mkaoni Arusha  kuwa na masuala ya Kidini wala Kisiasa.
Balozi Seif ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kuangalia mareruhi wa mlipuko huo waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuwapa pole Viongozi pamoja na waumini wa Kanisa lililopata maafa hayo.
Balozi Seif amesema Tukio hilo ambalo linadalili zote za Kigaidi limeshitua Taifa na kuwakera Wananchi wote  Tanzania Bara na Zanzibar na linafaa kulaaniwa na wapenda amani wote popote walipo.
Amefahamisha kwamba hiyo ni fitna inayojengwa katika kuleta chuki baina ya Serikali na Wananchi hasa waumini, hivyo amewasihi Watanzania kuendelea  kutulia na wala hakuna haja ya kuanza kutuhumiana ndani ya kipindi hichi kigumu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake kufuatia vyombo vya ulinzi kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wahusika wa mlipuko huo wapatao 10 hadi hivi sasa ambao kati yao wanne ni raia wa Saudi Arabia na Mmoja ni Raia wa Kenya.
Balozi Seif amewahakikishia wananchi wote pamoja na waumini  walioathirika na tukio hilo kwamba Serikali itahakikisha inawashikilia wale wote waliohusika na njama hizo na kuwachukulia hatua za kisheria kutokana na udhalimu wao huo.
Akizungumzia suala la Kidini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  amesema Serikali zote mbili zimetoa uhuru wa kuabudu ambao umo ndani ya katiba na kamwe haitavumilia kuona uhuru huo unaingiliwa na watu wachache.
Akitoa shukrani kwa niaba yake na waumini wenzake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Askofu Josephat Leburu amesema waumini wa jimbo hilo wamepata fafaja kubwa kufuatia ujio wa Viongozi mbali mbali wa Kitaifa waliofika kuwapa pole.
Askofu Josephat amesema moyo huu ulioonyeshwa na Vionmgozi wa Kitaifa umetoa sura sahihi uliyoonyesha ushirikiano wa karibu yao na Wananchi wanaowaongoza.
Hata hivyo Viongozi hao wa Kidini wameiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi kuendelea kutoa Taarifa kadri hatua zinavyochukuliwa za kukabiliana na tukio hilo waliloliita la kigaidi.
Wamesema hatua hiyo itasaidia sana kupunguza joto la waumini wao ambalo wakati mwingine hufiki maamuzi ya kutaka kuchukuwa hatua mikononi mwao wakati wanapokabiliwa na matukio  ya hujuma dhidi yao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nd. Nyerembe Munasa Sabi akitoa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto za waumini hao amesema Serikali Kuu kupitia, Mkoa na Wilaya hiyo inaendelea na juhudi za kuwasaka wale wote waliohusika la mlipuko huo.
Nd.  Nyerembe amefahamisha kwamba hadi sasa watuhumiwa kumi wameshatiwa mbaroni kwa msaada wa wananchi wema ambapo kati yao wanne ni raia wa Saudi Arabia na Mmoja Raia wa Kenya.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru ameeleza kwamba tukio hilo la mlipuko ni ishara ya ugaidi unaojenga chuki ambao umeandaliwa katika mazingira ya kitaalamu zaidi.
Amewasihi Viongozi na Waumini wa Kikristo  Mkoani humo kuendelea kuwa wastahamilivu wakati Serikali kuu inajitahidi kujenga mazingira yatakayosaidia kuepusha mgawanyiko miongoni mwa Wananchi.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kuwa hadi sasa Mlipuko huo ulisababisha vifo vya watu watatu, na wengine 66 kujeruhiwa ambapo mpaka muda huu watu 24 wamesharuhusiwa kurejea nyumbani na wengine 34 wanaendelea kupata huduma katika Hospitali ya Mkoa ya Arusha.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...